3 Februari 2021 - 12:10
Kashfa nyingine ya polisi ya Marekani

Serikali ya Mexico imetangaza habari ya kutiwa nguvuni maafisa 12 wa polisi ya Marekani kwa tuhuma za kuwaua wahamiaji 19.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Akizungumza na waandishi habari jana Jumanne, Irving Barrios, mwendesha mashtaka wa jimbo la Tamaulipas lililoko kaskazini mwa Mexico amesema kwamba polisi wasiopungua 12 wa Marekani wametiwa nguvuni kwa tuhuma za kushiriki katika mauaji ya wahajiri 19 wakiwemo raia wa Guatemala, kutumia vibaya madaraka na kutoa ripoti za uongo kwa maafisa wa Mexico.

Irving Barrios, amesema miili ya wahajiri hao ilipatikana katika magari mawili yaliyokuwa yameteketezwa moto tarehe 23 Januari mwaka huu wa 2021 katika barabara iliyoko karibu na mji wa Camargo unaopakana na jimbo la Texas nchini Marekani.

Uchunguzi wa awali umethibitisha kwamba wahajiri hao walipigwa risasi kabla ya miili yao kuchomwa moto kwenye magari hayo. Inasemekana kuwa wengi wa abiria waliokuwa kwenye magari hayo walikuwa wahamiaji waliokuwa wakijaribu kuingia Marekani.

Donald Trump rais wa zamani wa Marekani alikuwa mpinzani mkali wa kuingia nchini humo  wahamiaji kutoka nchi nyingine. Ni kutokana na upinzani huo mkali ndipo mwaka 2017 akaamuru ukuta ujengewe kwenye mpaka wa nchi hiyo na Mexico ili kuzuia wahajiri kutoka Mexico na nchi nyingine za Amerika ya Latini kuingia katika ardhi ya Marekani.

Msimamo mkali wa rais huyo wa zamani wa Marekani kuhusu wahamiaji na hatua yake ya kuwatenga watoto na wazazi wao wahamiaji hasa mwaka 2018 iliamsha hasira kali ya jamii ya kimataifa.

Hii ni katika hali ambayo Joe Biden, rais mpya wa Marekani ameanza uongozi wake nchini humo kwa kutupilia mbali siasa za Trump kuhusu suala zima la wahajiri na wahamiaji.

342/